• TANZAKILIMO TANZANIA

    Pata taarifa sahihi kuhusu kilimo na ufugaji,kwa weledi wa hali ya juu

  • WATAALA WA KILIMO NA UFUGAJI

    Tunakupatia ushauri wa kitaalam katika maswala yote ya kilimo na ufugaji,toka kwa wataalam wetu waliobobea kwenye nyanja nzima ya kilimo. Wasiliana nasi kwa simu namba +255 675 117 151.

  • UNATAFUTA MASOKO YA MAZAO YAKO? UNATAFUTA MAZAO YA KUNUNUA?

    Tanzakilimo inakuunganisha na wakulima/wanunuzi na wadau wote wa maswala ya kilimo. Wasiliana nasi leo tukuunganishe na wadau....

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo ujasiriamali. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo ujasiriamali. Onyesha machapisho yote

Ijumaa, 7 Septemba 2018

FAIDA NA HASARA ZA KUTUMIA KILIMO CHA GREEN HOUSE


GREEN House, kwa tafsiri isiyo rasmi, ni nyumba kitalu. Nyumba ambayo imejengwa kukidhi mahitaji ya mimea. Nyumba hizi hujengwa kwa ustadi mkubwa wa kitaalumu kwa kuzingatia baadhi ya mambo muhimu.

Baadhi ya mambo hayo muhimu ni pamoja na hali ya hewa ya eneo husika joto, baridi, mwanga wa jua, uelekeo wa upepo, muinuko kutoka usawa wa bahari, aina ya udongo, ubora wa maji, mteremko wa eneo husika.

Lakini pia kuna mambo ya kuzingatia kama aina za malighafi za kutumika na ubora wake nailoni, neti kivuli, mbao au chuma, plastiki, upatikanaji wa maji, kufikika kwa eneo, muinuko wa jengo (Gutter height), ni muhimu kuzingatia urefu kutoka usawa wa ardhi kabla ya kuezeka green house

Mazao yanayooteshwa kwenye mfumo huu yako ya aina maalumu kwa maana ya aina ya mbegu za kutumika/hybrid/F1, zenye sifa mbalimbali kama urefu, ipo namna yake ya uwekaji mbolea, kumwagilia ambazo ni njia tofauti sana na inavyofanyika katika mashamba ya wazi.

Sababu za watu kupenda kutumia aina hii ya kilimo

Kwanza kabisa sababu kubwa inayowasukuma wengi kuingia katika kilimo hiki ni ile ya kutoa mavuno mengi katika eneo dogo, kwa mfano kuna taarifa ambazo huenezwa na watu kuwa unaweza kupata tani 60 za zao kama nyanya ndani ya green house kwa eneo la upana wa mita 8 na urefu wa mita 15.

Aina hii ya taarifa ni moja ya kichocheo ambacho huwavutia sana watu, kwani mtu hupiga haraka hesabu za mapato na kuona kuwa inalipa.

Pia taarifa nyingine ambazo huwatia watu faraja na matumaini juu ya kilimo hiki ni kwamba ni aina ya mfumo ambao hauna usumbufu badala yake mtu hujipatia fedha zake kwa haraka.

Ukiacha taarifa za namna hiyo pia zipo zile zinazosema kuwa ukimaliza kujenga tu jengo la Green House, basi wewe ni tajiri yaani utakuwa na kazi ya kupanda na kusubiri kuvuna tu hata kwa miaka 10 mfulululizo.

Kwa taarifa kama hizi hufanya mtu kuwaza mapato makubwa, kuwa ikiwa kwa labda miezi 3 tu nina tani 60 za nyanya kwa eneo la mraba la mita 120, na anaambiwa unavuna tu, na jengo ni imara linadumu kwa miaka 10 bila matengenezo wala marekebisho.

Pamoja na kwamba aina hii ya kilimo imekuwa na faida lakini pia imekuwa na changamoto zake zinazowakumba wakulima wanaotumia mfumo huu wa kilimo.

Kwa maeneo ya miji mikubwa kama, Dar es Salaam na mikoa mingine zipo baadhi ya green house ambazo zimejengwa mwaka jana, lakini wamiliki wake wamezitelekeza na wengine wamezibomoa baada ya kuona wanapata mashambulizi ya magonjwa na wadudu.

Wapo baadhi ya wakulima kwa kupata taarifa zisizo sahihi waliaminishwa kuwa hakuna magonjwa wala wadudu wanaoshambulia mazao yaliyopo ndani ya green house, hivyo wakulima wakaishi kwa kujiamini kwa kujua kuwa wanachosubiria ni mapato ya tani 60.

Matokeo yake wamejikuta wanapata magonjwa na wadudu kama mazao ya shamba wazi, unakuta ni green house ya nyanya lakini ndani unakuta kuna changamoto ya wadudu.

Kuna baadhi ya wakulima mazao yao yamenyauka na kufa yakiwa ndani ya green house, kuna wakulima walijenga green house kwa matumaini ya kupata pesa ya haraka na wameishia kupata hasara kwa kuwa hawakupata ushauri sahihi na mazao yao yamekauka pia kama vile yapo kwenye shamba la wazi.

Mara nyingi green house hizi zimekuwa kwenye eneo lenye joto kubwa ikilinganishwa kuwa kimo chake kinapaswa kuwa chini ya mita 2.5, hivyo kufanya joto kuwa kali sana na mazao kunyauka, ambapo wataalamu wanashauri kuwa ni bora zaidi kujengwa kulingana na mazingira ya eneo au mkoa husika.

Mavuno kidogo.

Wapo wakulima waliolima ndani ya green house, mbali ya kwamba walikuwa wakiaminishwa kuwa watapata mavuno mengi yatakayowafanya kurudisha gharama zao ndani ya msimu mmoja matokeo yake imekuwa kinyume kabisa (mavuno hafifu na yasiyo bora) jambo ambalo linatokana na kutozingatia kanuni bora za uandaaji wa aina hii ya kilimo.

Kukosekana kwa soko

Baadhi ya wakulima waliowekeza kwenye kilimo hiki wamekuwa wakiaminishwa kuwa kwa kuwa ni mavuno ya green house, basi yatapata soko zuri muda wowote atakaovuna, jambo ambalo ni kinyume ambapo kwa sababu hizo wamekuwa wakizalisha mazao bila ya kuwa na hofu ya kukosa soko.

Na hivyo kujikuta kwamba pindi inapofikia wakati wa mavuno imekuwa kilio kwani mazao hayo yamekuwa yakipata bei sawa tu na yale ya mashamba ya kawaida huku wakati mwingine mazao hayo yakiharibika kabisa kwa kukosa soko.

Ubora hafifu wa mazao

Kwa mujibu wa wataalamu wanabainisha kuwa mazao huwa si mazuri na kutofanana hatua zote za ukuaji.

Kwani baadhi ya wakulima waliaminishwa kuwa mazao yote yaliyomo ndani ya green house yatakuwa katika kiwango sawa na yatafanana kwa kuwa yapo katika mazingira mazuri ya aina moja.

Hivyo kumfanya mmiliki kuamini kuwa kwa kuwa ni green house ni lazima ukuaji uwe bora na mzuri, hata kama hatofanya jitihada zozote, yeye atasubiri kuvuna na kupata pesa tu.

Ili kuweza kufanikiwa kwenye kilimo hiki cha green house basi kuna mambo ya kuzingatia kabla ya kuingia katika aina hii ya kilimo.

Wataalamu wa kilimo hiki wanasema kuwa kwanza kabisa ili mtu aweze kufanikiwa basi hana budi kuhakikisha kuwa anaweka juhudi, umakini na malengo katika jambo husika, kwani unaweza kuwa na green house lakini bado ukaambulia hasara na usifaidike na chochote kinyume na matarajio yako.

Na hivyo kwa sababu hiyo ukajikuta uko sawa tu kama siyo nyuma ya yule aliyelima kilimo cha kawaida ambacho ni cha wazi.

Lakini pia jambo jingine la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa unafahamu vizuri kilimo hiki, ikiwamo pia kutambua mbegu zilizobora na zinazoendana na soko unalolilenga kwani kinyume na hivyo unaweza kujikuta unaambulia hasara.

Hivyo ni busara kabla ya kuanza aina hii ya kilimo ni vizuri iwapo utatafuta ushauri kwa watu waliokwisha kufanikiwa kupitia mfumo huu lakini pia kutafuta taarifa mbalimbali juu ya aina hii ya kilimo.

Hii itakusaidia kujua changamoto na namna gani unavyoweza kuzikabili ikiwamo, gharama, magonjwa kwani usipokuwa makini unaweza kujikuta unakabiliana na changamoto zilizoko kwenye kilimo cha kawaida cha shamba wazi ilihali una green house.

Pia jambo jingine la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa unafanya utafiti wa kina kabla ya kuamua kuingia kwenye aina hii ya kilimo, hii itakusaidia kuweza kulibaini soko linavyokwenda na upande na kuvuna wakati gani.

Pia hakikisha kuwa unapata fundi ambaye ni mzoefu kwenye uandaaji huu wa green house ikiwamo kujiridhisha kwanza kuhusu ubora wa kazi zake alizowahi kufanya kabla ya kuingia makubaliano ya kukutengenezea green haouse yako.

Jumanne, 23 Mei 2017

Mtaji wa kufuga kuku wa kienyeji, mchanganuo wake na namna ya kupata soko


Pengine umekuwa ukiwaza sana nini ufanye ili uweze kufanikiwa na kuondokana na adha za umaskini. Yako mambo mengi ya kufanya mimi nataka kukufungua macho kwa jambo moja tu tena kwa uchache. Jambo hili anaweza kulifanya mwenye mtaji mkubwa au mdogo.
Somo langu ni dogo lakini naamini wapo watakaopata mafanikio makubwa sana. Sasa kuwa makini zaidi.

Unaweza kuanza kwa mtaji wa Mil.1 mpaka laki tano au hata chini ya hapo.

 

Mfano. Unaweza kutumia Tsh 250,000 kununua kuku 25 kwa bei ya Tsh 10,000 kwa kuku mmoja (kadirio la juu) Majogoo watakuwa 5 kwa uwiano wa 1:4.

Hii ina maana kuwa wakishaanza kutaga utakuwa na

 

vifaranga 20 x 10 = 200 Watunze vizuri.

 

Wale vifaranga tunakadiria kuwa makoo(majike) watakuwa 150 ambao ndani ya miezi 3 au zaidi nao wataanza kutaga.

 

Utakuwa na kuku 200 + 25 =225 ndani ya miezi 6. Miezi 6 inayofuata 225 - (majogoo 55) = 170 Hii ina maana kuwa 170 x 10= 1,700.

Ndugu mfuatiliaji, hayo niliyotoa ni makadirio ya chini sana hivyo mpaka mwisho wa mwaka utakuwa na kuku zaidi ya 2000. Mwaka utakaofuata utakuwa na kuku wangapi baada ya kuuza kuku 1,000. Miaka 2. 750(majike) x 10 = 7500 (uza wengine) 3000 x 10 = 30,000. Kutegemea na uwezo wako mpaka mwisho wa mwaka wa pili utakuwa umefanikiwa sana.

Kumbuka huu ni mwongozo tu, fanya utafiti na ufuatilie zaidi.

 

  1. Kumbuka kuku ninao wazungumzia hapa ni wale wa kawaida wa kienyeji.Fuatilia zaidi kuhusu matibabu na matunzo mengineyo.


.

A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?

  1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
    2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
    3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
    4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
    5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.


B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.

Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku

C:MAPUNGUFU

Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.

 

D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI

Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:

  1. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
    b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
    c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
    d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
    Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.


Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.

(i)          KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache mwilini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Zanzibar.

(ii) CHING'WEKWE

Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa sana kwa biashara ya mayai.

(iii)UMBO LA KATI

Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease)
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.

(iv) SINGAMAGAZI

Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.

(v) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49

(vi) PEMBA
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42

(vii) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6, mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.