• TANZAKILIMO TANZANIA

    Pata taarifa sahihi kuhusu kilimo na ufugaji,kwa weledi wa hali ya juu

  • WATAALA WA KILIMO NA UFUGAJI

    Tunakupatia ushauri wa kitaalam katika maswala yote ya kilimo na ufugaji,toka kwa wataalam wetu waliobobea kwenye nyanja nzima ya kilimo. Wasiliana nasi kwa simu namba +255 675 117 151.

  • UNATAFUTA MASOKO YA MAZAO YAKO? UNATAFUTA MAZAO YA KUNUNUA?

    Tanzakilimo inakuunganisha na wakulima/wanunuzi na wadau wote wa maswala ya kilimo. Wasiliana nasi leo tukuunganishe na wadau....

Jumamosi, 27 Mei 2017

Black Australorp ( Kuku Weusi wa Malawi)


Australorp wanastahimili mazingira tofauti, kama kuku wa kienyeji aliye zoeleka nchini Tanzania. Na ni wazuri kwa ufugaji huria, kwa kuwaachia nje wajitafutie chakula wenyewe. Ingawa wanajulikana kwa sifa yao ya utagaji mayai mengi, lakini kuku hawa wanafaa kwa nyama pia, kwani huwa na nyama nyingi sana (dual purpose chickens)

Kuku hawa huweza kumpatia mfugaji faida kubwa, kwani ni wazuri kwa biashara ya mayai na nyama pia. Hawana sifa nzuri ya kulalia mayai, lakini akilalia hutotoa vifaranga vingi, na ni wazuri kwa uleaji wa vifaranga hivyo.

Utagaji wao wa mayai unakaribia ule wa kuku wa kizungu. Kuku hawa ni wakubwa, wazito, na wanamvuto sana kuwaangalia. Wanapendeza pia kwa ufugaji mdogo, katika mazingira ya nyumbani. Wana michirizi ya kijani pale wanapomulikwa kwenye mwanga mkali wa jua.

Kwa wastani Black Australorp, hufikisha mayai 250 kwa mwaka, wakiwa katika mazimgira mazuri. Kuku hawa ni wapole na rafiki kwa binadamu. Black Australorp ni wagumu, hawapati magonjwa mara kwa mara, hivyo basi huvumilia magonjwa ya aina nyingi, na hawachagui chakula. Wanakula vyakula wanavyo kula kuku wengine wa kienyeji. Huanza kutaga wakiwa na umri wa miezi mitano na nusu hadi sita.

Jogoo hufikisha kilo 3.5 – 5.0 na
Temba/hen hufikisha kilo 3.0 – 3.7

kwa mahitaji ya aina hii ya kuku,wasiliana nami kwa simu namba o716 71729o,tuko kigamboni,dar es salaam

Jumatano, 24 Mei 2017

LISHE YA KUKU NA KUCHANGANYA CHAKULA


LISHE YA KUKU:

Ili kuku waweze kuishi, kukua vizuri, kunenepa na kutaga mayai mengi ni lazima wale chakula kingi na chenye ubora unaotakiwa. Uwingi na ubora wa lishe ya kuku unaweza kuainishwa katika makundi ya vyakula kama ifuatavyo:

  1. Vyakula vya kutia nguvu

  2. Vyakula vya kujenga mwili

  3. Vyakula vya kuimarisha mifupa

  4. Vyakula vya kulinda mwili

  5. Maji.


MAKUNDI YA VYAKULA:





    1. Vyakula vya kutia nguvu:




Vyakula vya mifugo vifuatavyo vinawekwa katika kundi hili;

  1. Pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano.

  2. Nafaka kama vile mtama , chenga za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi

  3. Mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi. Kabla ya kulisha kuku hakikisha mizizi hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili imo katika vyakula vya aina hii.Inashauriwa kuwamizizi hiyo ilishwe kwa kiasi cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.


Katika kundi hili la kutia nguvu ,vyakula vya mafuta kama vile mafuta ya kutoka kwenye vyakula vya mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kutia nishati huchangia asilimia 60-70 ya mchanganyiko wote wa chakula.

  1. Vyakula vya kujenga mwili:


Ø  Mashudu :Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula v vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya ,korosho, na ufuta .

Ø  Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), hii inafanywa ili kuepusha uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukiza .

Ø  Mabaki ya samaki ya samaki/dagaa na nyama.

Ø  Vyakula asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, Masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.

Ø  Vyakula hivi huchangia asilimia 20 hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.

  1. Vyakula vya kuimarisha mifupa(madini): a)Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kuuweka mwili wa ndege (kuku) katika hali ya afya njema kwa ujumla.

  2. b) Madini ya muhimu ni madini ya chokaa (calcium) na fosiforasi (phosphorus). Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa maganda ya konokono na mayai yaliyosagwa vizuri. Lakini inapendekezwa kwamba unapoongeza madini ya fosforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyopasa ,kwasababu kiwango cha aina moja kikizidi kuliko cha aina nyingine husababisha upungufu wa kile kidogo


Viinilishe vya madini vinavyotakiwa ni pamoja na;

Ø  Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa . Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vijidudu vya maradhi.

Ø  Chumvi ya jikoni

Ø  Madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate

Ø  Magadi (kilambo).

  1.     Vyakula vya kulinda mwili:


Kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;

Ø  Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, Chinese kabeji n.k.

Ø  na Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).

Ø  Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamini A na D zinatumika vizuri mwilini, kwahiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao unaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.

Ø  Chakula cha kuku wanaofugwa ndani ni lazima kichanganywe na vitamini zinazotayarishwa viwandani.

          KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:


Njia za kuchanganya chakula cha kuku;

Kuna njia kuu mbili za kuchanganya chakula cha kuku, nazo ni;

Ø  Kuchanganya chakula kwa mashine;

o   Njia hii hutumika viwandani kuchanganya chakula kwa ajili ya kuku wanaofugwa katika mashamba makubwa.

Ø  Kuchanganya chakula majumbani (home made ration): Hii ni njia inayotumika kuchanganya chakula kwa ajili ya kulisha kundi dogo la kuku na njia ambayo inaweza kutumiwa na wafugaji wadogowadogo.

VIFAA; Beleshi /koleo(spade), Turubai/sakafu safi, Viinilishe , Viroba/Magunia kwa ajili ya kuhifadhia chakula kilichochanganywa.

Chakula kilichochanganywa kinaweza kuwekwa katika uzani wa kilo 25-kilo 50, au kilo 100.

                MCHANGANUO WA VIINILISHE VYA CHAKULA CHA KUKU:

 

Aina ya chakula                                   kiasi

  1. Vyakula vya kutia nguvu mwilini:


Ø  Pumba za mahindi            kilo   48

Ø  Pumba laini za mpunga    kilo   26

            Jumla                                            kilo 74

  1.      Vyakula cha kujenga mwili : 


                                       

    MASHUDU YA ALIZETI                                   KILO 18


Damu ya wanyama                                                                    kilo   1

Mabaki ya samaki /dagaa                                                          kilo   3

          JUMLA                                              KILO  22


iii.Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini):

  1. chumvi ya jikoni                                   kilo ½

  2. chokaa(dicalciumphosphate)…            kilo 2

  3. poultry premix/                                     kilo ½

  4.  unga wa mifupa                                  kilo 1


          Jumla                                                      kilo 4

  

Ø  Mahitaji halisi ya viinilishe kwa muhtasari:

Ø  Vyakula kutia nguvu mwilini                             kilo 74

Ø  Vyakula vya kujenga mwili                              kilo 22

Ø  Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini)        kilo 4

  JUMLA                                                                        100

Jumla ya mchanganyiko wa vyakula                kilo 100 

 


HATUA ZA KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:


HATUA YA KWANZA:

Katika hatua ya kwanza utaanza kuchanganya vyakula vya madini

Changanya , chokaa, chumvi na majivu ya mifupa pig mix vizuri - huu utauita mchanganyo Na.1

HATUA YA PILI:

Changanya mchanganyo huo na damu pamoja na samaki waliosagwa - huu utauita mchanganyo Na. 2

HATUA YA TATU:

Mchanganyo Na.2 uchanganye na mashudu vizuri ambao utauita mchanganyo Na.3.

HATUA YA NNE:

Mchanganyo Na.3 umwage juu ya rundo la pumba iliyochanganywa (pumba ya mahindi na pumba laini ya mpunga).

o   Chukua beleshi /koleo safi lililo kavu na kulitumia kuchanganya rundo la chakula ili kusambaza viinilishe vizuri.

Mambo ya kuzingatia katika kulisha na kutunza chakula cha kuku:

  1. a) Baada ya kuchanganya chakula kitawekwa kwenye viroba au magunia na kutunzwa ghalani (stoo) hadi pale kitakapohitajika kwa ajili ya kulisha kuku.

  2. b) Hakikisha kuku wanapata lishe kadri inavyopendekezwa na wataalamu.

  3. c) Chakula kilichochanganywa ni lazima kiwekwe sehemu kavu ili kisiharibiwe na unyevunyevu kama vile kwenye chaga mabanzi yaliyotandazwa juu ya mawe yalipangwa vizuri

  4. d) Chakula kilichoharibika hakifai kulisha kuku kwani kinaweza kusababisha matatizo ya afya.

  5. d) Chakula kilichochanganywa kinatakiwa kisikae muda mrefu baada ya kutayarishwa.


Vyakula vya ziada:

Ili kuhakikisha kwamba kuku wanapata viinilishe vya kutosha kuku wanaweza kupewa mchwa na mafunza.

Vilevile vitu mbadala aina ya nafaka vinavyopatikana hutegemea sana aina ya mazao yanayolimwa katika eneo husika.

Mbinu za kuotesha mchwa na funza: Funza na mchwa ni chakula kizuri na rahisi chenye viinilishe aina ya protini kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo huria unaoboreshwa. Hata hivyo vyanzo hivi vya chakula cha protini huchangia tu vile ambavyo kuku wanatakiwa kupewa.

  1. Inashauriwa uwape vifaranga hao funza na mchwa kwa sababu ndio wanaohitaji protini kwa kiasi kikubwa na cha kuaminika.


Funza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa njia rahisi na kutumika kuboresha chakula cha vifaranga.

  1. c)Mafunza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa kutumia damu, viungo vya ndani ya tumbo la ng’ombe pamoja na samadi ya ng’ombe.

  2. d) Chungu kijazwe maji theluthi moja ya ujazo wake, inzi watakuja na kutaga mayai katika mchanganyiko ambao mafunza walioteshwa wataanza kula mchanganyiko huo.

  3. e) Baada ya hapo vitu hivi vyote vitachanganywa pamoja katika chungu kimoja kikubwa ambacho kitaachwa wazi wakati wa mchana na kufunikwa wakati wa usiku.

  4. f) Siku tano baadaye maji yatajazwa kwenye mtungi huo na mafunza yatakusanywa wakiwa wanaelea juu. Baada ya kukusanya waoshe vizuri na maji halafu lisha kuku moja kwa moja.

  5. g) Kumbuka kuweka chungu kinachooteshwa mafunza kuweka mbali na maeneo ya watu ili kuepuka harufu inayoweza kusumbua watu.


                                                  KULISHA KUKU:  
 

Makadirio ya chakula cha kuwalisha vifaranga 100/siku moja:






































Umri (wiki baada ya kuzaliwa)Idadi ya

vifaranga
Kiasi kinachotakiwa

Kwa siku moja(kilo)
11001
21001
31002
41003
51004
61005

Maelezo kwa ufupi  kuhusu kulisha kuku:

  • Ni vigumu kukadiria mahitaji ya chakula cha kuku wanaojitafutia chakula, lakini inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani lakini wale kuku wanafugwa kwa mfumo wa huria nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .

  • Ifahamike pia kuwa kiasi cha chakula hutegemea mahitaji kutokana na uzito na uzalishaji, mfano kuku anayetaga na anayekua wanahitaji chakula kingi zaidi ya wale ambao hawatagi au wamekoma kukua.

  • Hakikisha kuku wanawekewa chakula na maji safi kwenye vyombo safi na kubadilisha kila vitakapoisha.

Jumanne, 23 Mei 2017

Mtaji wa kufuga kuku wa kienyeji, mchanganuo wake na namna ya kupata soko


Pengine umekuwa ukiwaza sana nini ufanye ili uweze kufanikiwa na kuondokana na adha za umaskini. Yako mambo mengi ya kufanya mimi nataka kukufungua macho kwa jambo moja tu tena kwa uchache. Jambo hili anaweza kulifanya mwenye mtaji mkubwa au mdogo.
Somo langu ni dogo lakini naamini wapo watakaopata mafanikio makubwa sana. Sasa kuwa makini zaidi.

Unaweza kuanza kwa mtaji wa Mil.1 mpaka laki tano au hata chini ya hapo.

 

Mfano. Unaweza kutumia Tsh 250,000 kununua kuku 25 kwa bei ya Tsh 10,000 kwa kuku mmoja (kadirio la juu) Majogoo watakuwa 5 kwa uwiano wa 1:4.

Hii ina maana kuwa wakishaanza kutaga utakuwa na

 

vifaranga 20 x 10 = 200 Watunze vizuri.

 

Wale vifaranga tunakadiria kuwa makoo(majike) watakuwa 150 ambao ndani ya miezi 3 au zaidi nao wataanza kutaga.

 

Utakuwa na kuku 200 + 25 =225 ndani ya miezi 6. Miezi 6 inayofuata 225 - (majogoo 55) = 170 Hii ina maana kuwa 170 x 10= 1,700.

Ndugu mfuatiliaji, hayo niliyotoa ni makadirio ya chini sana hivyo mpaka mwisho wa mwaka utakuwa na kuku zaidi ya 2000. Mwaka utakaofuata utakuwa na kuku wangapi baada ya kuuza kuku 1,000. Miaka 2. 750(majike) x 10 = 7500 (uza wengine) 3000 x 10 = 30,000. Kutegemea na uwezo wako mpaka mwisho wa mwaka wa pili utakuwa umefanikiwa sana.

Kumbuka huu ni mwongozo tu, fanya utafiti na ufuatilie zaidi.

 

  1. Kumbuka kuku ninao wazungumzia hapa ni wale wa kawaida wa kienyeji.Fuatilia zaidi kuhusu matibabu na matunzo mengineyo.


.

A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?

  1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
    2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
    3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
    4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
    5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.


B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.

Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku

C:MAPUNGUFU

Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.

 

D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI

Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:

  1. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
    b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
    c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
    d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
    Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.


Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.

(i)          KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache mwilini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Zanzibar.

(ii) CHING'WEKWE

Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa sana kwa biashara ya mayai.

(iii)UMBO LA KATI

Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease)
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.

(iv) SINGAMAGAZI

Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.

(v) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49

(vi) PEMBA
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42

(vii) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6, mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.

Jumamosi, 13 Mei 2017

Dume Mzuri Kwa Uzalishaji Wa Ng’ombe Wa Maziwa


http://ufugajimakini.blogspot.com/

Tunaangalia uchaguzi wa dume mzuri kwa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, pamoja na aina ya malisho ambayo mfugaji anaweza kuyatumia kuweza kukabiliana na changamoto ya malisho kwa ng’ombe.
Wafugaji wengi wamekuwa wakipata ng’ombe wanaozalisha kidogo na kwa kiwango cha chini kutokana na kuangalia ukubwa wa gharama ya mbegu wakidhania kuwa ndiyo upatikanaji wa ng’ombe bora. Vinasaba husaidia kwa kiwango kikubwa katika kupata ng’ombe mzuri wa maziwa.



http://ufugajimakini.blogspot.com/

Kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa maziwa hutegemeana na vitu viwili ambavyo ni kuboresha mifugo kwa kufanya uchaguzi sahihi wa kizazi pamoja na usimamizi mzuri unaojumuisha lishe kamili, malazi mazuri, upatikanaji wa maji,kuwa karibu na wanyama pamoja na utoaji wa kinga na tiba dhidi ya magonjwa.



Vinasaba pamoja na usimamizi mzuri ni vitu viwili vinavyotegemeana. Bila kuwa na uzao mzuri, uzalishaji wa wanyama pamoja na usimamizi utakuwa wa hali ya chini sana, na bila usimamizi mzuri wanyama bora hawawezi kuonesha ubora wao katika uzalishaji.



Uzao mzuri humpa nafasi kubwa mfugaji kutambua sifa na uzalishaji utakaopatikana katika uzao ujao. Endapo mfugaji atafanya uchaguzi mbaya basi ni hakika atakuwa na uzalishaji hafifu wa maziwa, kuzorota kwa afya ya mnyama pamoja na maisha mafupi.



Muda wa kufanya tafiti



Wafugaji wengi wamekuwa wakifikiria mbegu pale tu ng’ombe anapokuwa tayari anahitaji kupandwa na matokeo yake ni kuwa, kutokana na haraka ya kutaka kumhudumia ng’ombe huyo, basi mfugaji atakuwa tayari kuchukua mbegu yoyote ile atakoyopatiwa na wataalamu. Kwa mantiki hiyo, hakuna muda mfugaji atatumia kuchunguza aina ya dume aliyetumika kupatikana kwa mbegu hiyo na badala yake, gharama hutumika kwa kiasi kikubwa kuonesha uwezo wa dume huyo.



Wafugaji wengi hufikiri kuwa kitendo cha mbegu kuuzwa kwa gharama kubwa ni moja ya njia ya kutambua ubora wa dume. Wauzaji wengi wamekuwa wakitumia njia hii kuwadanganya na kuwarubuni wafugaji.



Ni muhimu sana kwa mfugaji anaelenga kuzalisha maziwa kusoma na kuelewa taarifa zote muhimu zilizotolewa kuhusu aina ya dume husika. Ili kufanikiwa katika uzalishaji wa maziwa, ni muhimu kwa mfugaji kuwa makini na kulichukulia kwa uzito suala la uchaguzi wa dume na kuelewa nini kinahitajika bila kubahatisha. Mfugaji ni lazima atambue kuwa, dume huchangia asilimia 50 ya kinasaba katika uzao wake hivyo ni muhimu sana kujua sifa za dume unayemchukua kwa ajili ya uzalishaji. Pia ubora wa maziwa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya dume aliyetumika. Dume wa maziwa hutambulika kwa kuangalia kiwango cha maziwa yanayozalishwa na ng’ombe aliyepandwa na dume huyo na mtamba aliyezaliwa na ng’ombe huyo ambapo dume huyo husambaza sifa ya maziwa kutoka kwa ng’ombe huyo hadi kwa mtamba.



Elewa maelekezo yaliyopo kwenye kabrasha la mbegu



Kielelezo cha vinasaba hutumika kupima uwezo wa mnyama kusambaza vinasaba vyake kwenda kwa uzao ujao. Katalogi huwa na taarifa muhimu ambazo zitamsaidia mfugaji kufanya uchaguzi mzuri wa dume ili kuwa na uhakika wa kuendeleza kizazi baada ya kingine.